Na: Stella Mmbando - HAI
Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa amewataka wakuu wa idara na
watumishi wote wa Wilaya hiyo kujituma
na kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao idara zao ili kuongeza ufanisi
na kuimarisha ari ya kufanya kazi kwa maendeleo ya taifa.
Byakanwa alizungumza hayo wakati wa
kutoa tuzo za mshindi wa shindano la ubunifu kwa idara na vitengo vya
halmashauri hiyo ambapo mwezi huu zimeshindanishwa idara tatu ikiwamo idara ya mapato,
biashara na mazingira.
Idara ya biashara ndio iliibuka na ushindi kwa mwezi Septemba ikizibwaga idara za mapato na mazingira ambapo washindi wameonesha ubunifu wa hali ya juu katika kukusanya mapato ya leseni kupitia viongozi wa vijiji na kuwa wameshakusanya mapato ya zaidi ya shilingi milioni arobaini kwa kipindi cha miezi mitatu ikiwa ni sawa na asilimia hamsini ya lengo la idara kwa mwaka ambalo ni shilingi milioni themanini na mbili laki moja na tisini elfu huku wakibainisha kuwa bado zipo kata ambazo bado hazijafikiwa na uhamasishaji huo.
Imeelezwa mbele ya Mkuu wa Wilaya
na majaji wa shindano na watumishi wote wa halmashauri hiyo kuwa wafanyabiashara
mia nane walijitokeza kukata leseni za biashara ikiwa ni muitikio wa kampeni
kabambe iliyofanywa na washindi kupitia matangazo na kutoa elimu kwa kutumia
rediio inayomilikiwa na halmashauri.
Aidha kwa upande wao idara ya
mazingira wameonesha ubunifu kwa kukusanya pesa katika kituo cha kutupia taka
cha Tumaini, kuzalisha mbolea kutokana na taka pamoja na kukusanya na kuondoa
taka katika barabara zote zilizopo
wilaya ya Hai.
Shindano la ubunifu maarufu kama “Byakanwa
Awards” limeanzishwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai Gelasius Byakanwa kwa lengo la
kuinua ari ya utendaji miongoni mwa watumishi wa umma katika wilaya hiyo ambapo
kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi idara tatu zinawasilisha mbele ya majaji taarifa
ya utekelezaji wa majukumu ikionesha ubunifu uliotumika na mafanikio
yaliyopatikana huku wakitaja changamoto walizokutana nazo na namna
walivyozipatia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment