Friday, June 8, 2018

DC Awaasa Wanufaika TASAF Kujiunga na Bima ya Afya


Mkuu wa Wilaya ya Hai; Onesmo Buswelu akizungumza na baadhi ya wananchi wanaonufaika na Mradi wa Kunusuru Kaya Masikini unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) alipotembelea zoezi la kuhawilisha fedha kwenye Kijiji cha Tindigani. Kulia kwake ni Diwani wa Kata ya Kia; Yohana Laizer. (Picha zote na Adrian Lyapembile)



Na Adrian Lyapembile
HAI

MKUU wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Onesmo Buswelu amewataka wananchi wanaonufaidika  fedha zinzotolewa na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa ajili ya  kunusuru kaya masikini kutumia  sehemu ya fedha hizo na kujiunga na bima ya afya.Akizungumza na wananchi wanaonufaika na mpango huo wakati wa zoezi uhawilishaji wa fedha katika kijiji cha Tindigani aliwataka kuhakikisha kuwa  wanajiunga na Bima ya afya ili waweze kupata matibabu pindi wanapougua.


“Serikali imelenga kuboresha maisha ya wananchi wake, ni vyema ninyi mnaopata fedha za TASAF kuzitumia pia kwa kujikatia bima ya afya ambayo inawapa nafasi ya kutibiwa katika zahanati na vituo vya afya pamoja na hospitali ya wilaya kwa kupitia Bima hiyo ”amesema Buswelu.
“Unaweza ukaanza kutenga fedha kidogo kidogo kadiri unavyopata kwa kila awamu na hatimaye  ukafanikiwa  kupata fedha zitakokuwezesha kuwa na bima yako itakayokupa na nafasi wewe na familia yako kupata huduma kwa uhakika” amefafanua.


“Mtu  anaweza kupata maradhi muda wowote bila kujali kama ana pesa ama la lakini akiwa na bima ya afya anao uhakika wa kupata matibabu wakati wowote” amesisitiza.


Akizungumzia baadhi ya wanufaika kutumia fedha hizo kwa kununua pombe amesema kuwa serikali haitasita kuwaondoa  katika mpango kwani lengo la mpango huo ni kuhakikisha kuwa kila mmoja anabadili hali yake kiuchumi.


Kwa upande wake mtendaji wa kijiji hicho, Theodora Kessy amesema tangu mpango huo kuanzishwa umeleta mabadiliko makubwa kwani wanufaika wengi wameweza kuanzisha miradi midogo ikiwemo ufugaji wa kuku na mbuzi.


“Mpango huu umeboresha mahudhurio ya wanafunzi  shuleni , pia umechangia mwitikio kwa wanawake wenye watoto wadogo kuhudhuria kiliniki kama inavyotakiwa” alisema.


Naye Diwani wa kata ya Kia, Yohana Laizer aliwasisitiza wanufaika wa fedha hizo kutozitumia kwa matumizi ya kawaida badala yake wajitahidi kuanzisha miradi midogo watakayoweza kuimudu ili kujikomboa kiuchumi na kufanikisha lengo kuu la mradi huo.


“Mradi huu ni wa mda na ipo siku utafikia mwisho hivyo basi ni vyema kila mmoja wetu aliyepata bahati ya kunufaika akatumia mradi huu kwa malengo ya kujiinua kiuchumi ili mradi utakapofikia mwisho uwe na kitu cha kukusaidia kupata mahitaji yako ya muhimu” amesema Diwani huyo.


Wanufaika wa TASAF wakiwa wamejipanga nje ya ofisi ya Kijiji wakiendelea na zoezi la kujiandikisha na kujaza fomu 
Mnufaika wa Fedha za TASAF akijiandikisha mbele ya Mtendaji wa Kijiji cha Tindigani Theodora Kessy 

Zoezi la kuhawilisha fedha kwa wanufaika wa TASAF likiendelea katika kijiji cha Tindigani, Kata ya Kia Wilayani Hai


No comments:

Post a Comment