Monday, February 12, 2018

AFISA ELIMU AAGIZA KUANZISHWA JUKWAA LA WAZAZI SHULENI


Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Hai Julius Kakyama akisisitiza jambo kwenye kikao cha wazazi wa wanafunzi kwenye shule ya sekondari Hai. (Picha zote na Praygod Munisi)


Na. Praygod Munisi
HAI

Wakuu washule za sekondari za serikali katika wilaya  ya  Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuanzisha jukwaa la wazazi na walimu ndani ya mwezi mmoja ikiwa ni sehemu ya kutekeleza majukumu yao ili kutoa nafasi ya kujadiliana mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya shule na wanafunzi.


Agizo hilo limetolewa na Afisa Elimu sekondari wilaya ya Hai Bw. Julius Kakyama wakati akizungumza na wazazi katika kikao kilichofanyika katika shule ya sekondari Hai iliyopo mjini Bomang’ombe, ambapo amesisitiza ushirikiano kwenye jukwaa la wazazi na walimu na kuwataka kutumia jukwaa hilo kama sehemu sahihi ya kutatua changamoto zinazowakuta wanafunzi katika safari yao ya kutafuta elimu.
 

Wazazi wakimsikiliza kwa Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Hai Julius Kakyama (hayupo pichani) alipofanya kikao na wazazi wa wanafunzi kwenye shule ya sekondari Hai. (Picha na Praygod Munisi)

Kakyama amewakumbusha walimu kuwa na nidhamu na maadili ili wawe mfano mzuri wa kuigwa na wanafunzi wanaowafundisha na hatimaye kutengeneza taifa lenye watu waaminifu wenye nidhamu ambao watashiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya taifa lao.

Aidha Kakyama amewakumbusha wazazi kusimamia vizuri jukumu lao la malezi kwa wanafunzi wanapokuwa nyumbani kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya masomo ya watoto wao ikiwemo kuwapatia mahitaji yote muhimu kwa pamoja na kuhakikisha kuwa wanahudhuria shuleni huku wakiwalea watoto hao katika maadili mema wakishirikiana na walimu jambo ambalo litasaidia kupunguza changamoto za  utoro mashuleni lakini pia itasaidia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu.


Afisa Elimu Sekondari anafanya mikutano ya mara kwa mara na walimu pamoja na wazazi katika shule zilizopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambapo amekuwa akishiriki kujadili maendeleo ya elimu wilayani pamoja na kutoa tafsiri ya maelekezo ya serikali ikiwemo kutambua nafasi ya mwalimu, mzazi na mwanafunzi katika swala zima la elimu bila malipo.

No comments:

Post a Comment