Thursday, June 26, 2014

VIJIJI 11 WILAYANI HAI KUNUFAIKA NA UMEME WA REA


 
Zaidi ya vijiji 11 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro vikiwemo vijiji vya Mungushi, Mtakuja, Tindigani na Mlima shabaha vinatarajia kunufaika na  huduma ya umeme kupitia wakala wa umeme vijijini REA huku vijiji vitakavyofuatia mara baada ya kukamilika kwa awamu hiyo ni vijiji vya chemka, kambi ya nyuki, kilimambogo, mbatakero,pamoja na modio.

Hayo yamebainishwa  na meneja wa  Tanesco Wilaya ya Hai Bw. James Chinula wakati wa uwasilishaji wa mada katika kikao cha baraza la wafanyabiashara wilaya ya Hai

Chinula amesema kuwa baada ya kupatikana kwa substation mpya ya KIA na kukidhi mahitaji ya Wilaya ya Hai zaidi ya vijiji 11 vitapatiwa huduma hiyo kwa awamu ya kwanza.

Naye meneja wa TRA Wilaya ya Hai na Siha bw. Silver Rutagwelera amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2013/2014 zaidi ya shilingi billion 1.7 zimekusanywa kama mapato huku lengo la mwaka unaoanza ni kukusanya shilingi billion 2.2. 

katika hatua nyingine wafanyabiasha bw. Johnson Mtey  amesema kuwa elimu ya matumizi sahihi ya mashine za EFD itolewe ili kuondoa dhana iliyopo miongoni mwa wafanyabiashara juu ya matumizi ya mashine hizo jambo ambalo bw. Rutagwelera amesema kuwa mbali na semina zilizotolewa bado elimu zaidi inaendelea kutolewa.

Awali akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Hai ndugu Novatus Makunga  ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa baraza hilo amesema kikao hicho ambacho sasa kitakuwa kinafanyika mara kwa mara kimelenga kujadili fursa na changamoto za biashara zilizopo kwa lengo la kuimarisha na kukuza biashara na kuongeza ushirikiano baina ya sekta binafsi na sekta za Umma ili kuongeza ufanisi katika kazi.

habari imeandikwa na Gasper Mushi

No comments:

Post a Comment