HAI
Wananchi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuchangamkia
fursa za kiuchumi kwa kushiriki kwenye kilimo cha mazao ya biashara likiwemo zao
la korosho ambalo linastahimili hali ukame na kustawi kwenye mazingira ya ukanda wa tambarare wa Wilaya hiyo.
Zao hilo ambalo limetambulishwa kwa mara ya kwanza wilayani hapo kwa uzinduzi uliofanyika tarehe 17/05/2018 kwenye jengo la Kituo cha Rasilimali za Kilimo (WARC) lililopo kata ya Masama Rundugai.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa zao hilo; Katibu Tawala Wilaya ya Hai
Upendo Wella amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua miche inayogawiwa
bure na serikali lakini pia kutoa maeneo yao kwa ajili ya kuotesha miche ya korosho
kwani zao hilo ni moja ya mazao ya biashara yanayofanya vizuri kibiashara na
litasaidia sana katika kuinua uchumi wa wananchi hasa wa ukanda wa tambarare.
“Natoa wito wa serikali kwa wananchi wa maeneo yatakayolimwa zao hili wakiongozwa
na wenyeviti wa vijiji na viongozi wengine katika maeneo yao wahamasishane
kuendelea kutenga maeneo ya kuotesha miche ya korosho ili kufikia lengo la
kuotesha miche 5000 kwenye kila kijiji ili kuweza kuona tija na faida za zao
hili” Amesema Wella.
Katibu Tawala Wilaya ya Hai Upendo Wella akipanda mche wa korosho kuashiria uzinduzi wa zao hilo mara baada ya kulitambulisha rasmi kwa wakazi wa Wilaya ya Hai. |
Wella amewata wale watakaopatiwa miche inayogawiwa na serikali kuitunza
vizuri kwenye mashamba watakapoipanda kwani serikali imetumia fedha katika
kuandaa miche hiyo ili iweze kumfikia mwananchi bila gharama huku akiwaagiza
wataalamu wa kilimo kuwafikia wananchi kwa ajili ya kuwapatia elimu na usaidizi
wa kitaalamu wakati wa kutunza miti ya korosho kwa ajili ya kupata mavuno
makubwa zaidi.
Akitoa salamu za wilaya kwa mgeni rasmi; Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo amewapongeza wananchi wa kata ya
Masama Rundugai kwa namna wanavyolitunza na kulitumia jengo la Rasilimali za
Kilimo kwa ajili ya kupata elimu ya mambo yanayohusu kilimo.
Aidha Sintoo amewahimiza wananchi kuona umuhimu wa kulima zao la korosho
ambalo halina gharama kubwa katika matunzo lakini pia ni zao la muhimu katika
uchumi wa viwanda litakalobadilisha hali ya kiuchumi ya wananchi watakaolima
zao hilo.
“Leo tunazindua rasmi kilimo cha korosho kwenye ukanda wa tambarare wa
wilaya yetu; tuna furaha sana tumepata miche elfu 16 kutoka Bodi ya Korosho na
tumeona vema kwanza tufanye shamba darasa kwenye eneo la heka 2 za Shule ya
Msingi Rundugai litakalotumiwa na wataalamu wa kilimo kuwafundishia wakulima”
ameongeza Sintoo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masama Rundugai, Elibariki Mbise amewataka
wananchi kupokea vizuri zao la korosho kwenye maeneo ya ukanda wa tambarare
kwani ni sehemu ya kutunza mazingira lakini pia mavuno yatokanayo na zao hilo
yatasaidia kuboresha uchumi wa wakulima huku akihusisha kwa karibu zao hilo na
maendeleo ya viwanda.
“Zao hili lina manufaa makubwa mbali na kuwa ni zao kwa ajili ya biashara
lakini pia ni sehemu ya kuhifadhi na kutunza mazingira kama mti lakini pia
tumeona umuhimu wa zao hili kwa uchumi kwani bei ya kahawa na bei ya korosho
zinakaribiana. Sasa ukanda wa juu kahawa na ukanda wa tambarare ni korosho”
Amesisitiza Diwani Mbise.
Naye Afisa Kilimo wilaya ya Hai, David Lekei amebainisha sababu ya zao la
korosho kulimwa ukanda wa tambarare kuwa ni kwa sababu ukanda wa tambarare
unapata mvua kidogo na kukaa muda mrefu katika hali ya ukame kitu ambacho zao
la korosho linahimili.
Afisa Kilimo Wilaya ya Hai David Lekei akipanda mche wa korosho katika uzinduzi wa kilimo cha zao hilo katika shamba la Shule ya Msingi Rundugai. |
Lekei ameongeza kuwa hadi sasa yamepatikana maeneo ya kuotesha miche ya korosho
kwenye vijiji 23 vya kata tisa kukiwa na jumla ya hekari 643 zilizo tayari kwa
ajili ya kuotesha miche huku wakulima 450 wameshajitokeza kutaka kuotesha miche
ya zao hilo.
Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Rundugai walioshiriki kwenye uzinduzi huo wamesema wanafurahi kuona zao hilo limefika kwenye maeneo yao na wanategemea watafaidika na mavuno ya zao hilo katika kuboresha hali yao ya kiuchumi.
Bi. Mwanaisha Msuya akizungumza na waandishi wa habari kuelezea furaha yake baada ya kutambulishwa kwa zao la korosho katika Wilaya ya Hai. |
“Kwa jinsi tunavyosikia wenzetu wa Mtwara na Lindi wanavyopata mazao mengi inatupa moyo na sisi kuwa tutapata mazao kwa ajili ya biashara ila tunaomba serikali iendelee kutuelimisha kuhudumia zao hili kitaalamu” amesema Mwanaisha Msuya mkazi wa Rudugai.
Uzinduzi wa kilimo cha korosho katika ukanda wa tambarare wa wilaya ya
Hai mkoani Kilimanjaro umefanikiwa baada ya kukamilika kwa utafiti uliofanywa
na wataalamu na kuthibitisha kuwa maeneo hayo yanafaa kwa kilimo cha zao hili
huku ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ya serikali ya kufufua mazao makuu matano
ya kibiashara ya Pamba, Chai, Tumbaku, Kahawa na Korosho hivyo kufanya Wilaya
ya Hai kupata mzao makuu mawili ya Kahawa kwenye ukanda wa juu na korosho
kwenye ukanda wa tambarare.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Rundugai wakishiriki uzinduzi wa zao la korosho |
No comments:
Post a Comment