Friday, June 8, 2018

Serikali Yajipanga Kumaliza Mgogoro wa Muda Mrefu

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Onesmo Buswelu akisisitiza jambo kwenye mkutano na wananchi wa kijiji cha Tindigani alipofika kujadili namna serikali itakavyomaliza mgogoro wa mipaka ya kiwanja cha ndege cha KIA.   (Picha zote na Adrian Lyapembile)


Na Adrian Lyapembile
HAI

SERIKALI wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro imesema mgogoro kati ya wananchi wanaopakana na  kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) utatuzi wake utazingatia sheria  na kila mwananchi haki yake italindwa kwa mujibu wa sheria  za nchi.
Mkuu wa wilaya hiyo, Onesmo Buswelu, amesema serikali imeanza mchakato wa kumaliza mgogoro huo kupitia kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria katika kumaliza mgogoro  huo uliyodumu kwa zaidi ya miaka kumi.
Akizungumza  na  wananchi katika ziara yake kwenye vijiji  vitano vinavyohusika na mgogoro huo, Buswelu amewataka kuwa na subira wakati huu ambapo serikali inaendelea kutafuta  suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.
Buswelu amesema serikali itafanya kazi ya kuweka alama za  kutambua mipaka halisi ya maeneo ya kiwanja hicho ili kuweza kuwatambua  wananchi ambao watakuwa ndani ya eneo linalomikiwa na kiwanja hicho kwa ajili ya kuendelea na hatua za ufumbuzi.
“Nchi yetu inaongozwa na kuheshimu sheria. Utatuzi wa mgogoro huu utazingatia sheria na kila mwananchi afahamu kuwa haki yake italindwa kwa mujibu wa sheria; kama mtu anayo haki ya kulipwa basi atalipwa kwa mujibu wa sheria”alisema Buswelu
“Mgogoro huu wa  wananchi wanaopakana na kiwanja hicho umedumu kwa muda mrefu kiasi cha kuwepo hali ya sintofahamu miongoni mwa wananchi hao hasa pale wanapotakiwa kusitisha uendelezaji wa maeneo yao kwa kuweka majengo ya kudumu kama nyumba, zahanati, shule za kudumu hali ambayo imewafanya wananchi kulalamikia serikali lakini kwa sasa tunatafuta ufumbuzi wa kudumu ni vema mkawa na subira”alisisitiza Mkuu huyo wa wilaya.

Akizungumzia hatua ya serikali kumaliza mgogoro afisa kutoka Wizara ujenzi, Mawasiliano na uchukuzi, sekta ya viwanja vya ndege, Mhandisi Rogatus Matigira alisema zoezi la kupima maeneo ya kiwanja na kuweka alama litasaidia kufahamu ukubwa wa tatizo na kufahamu idadi ya wananchi walio ndani ya maeneo ya kiwanja cha ndege lakini pia itasaidia.
“Serikali baada ya kuwa na huu mgogoro muda mrefu wa mipaka kati ya Uwanja wa KIA na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani; imeona iangalie ukubwa wa tatizo kwa kupima na kuweka alama ndipo ifanye maamuzi huku ikitumia maeneo ya kia kama rejea itakayosaidia kujua walioko ndani na nje ”.

Diwani wa Kata ya Kia, Yohana Laizer akichangia mada kwenye mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Hai walipokuwa wakijadili namna ya kumaliza mgogoro wa mipaka ya kiwanja cha ndege cha KIA.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kia,Yohana Laizer ameiomba serikali kutumia hekima na busara kutafuta namna ya kunusuru maeneo ya wananchi huku akikumbusha kuwa vijiji vya vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria lakini pia wao kama wananchi hawana uwezo wa kuitunishia serikali.
Vijiji vinavyohusika na mgogoro wa mipaka na uwanja huo ni Chemka,Rundugai, Sanya Station, Tindigani na Mtakuja ambavyo vipo katika kata ya Masama Rundugai na Kia. 

Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Tindigani Wilaya ya Hai Wakifuatilia mkutano wa Mkuu wa wa Wilaya hiyo 

No comments:

Post a Comment