Monday, June 16, 2014

HOTUBA YA MGENI RASMI-NDUGU FAISALI ISSA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA NA UZINDUZI WA KITUO JUMUISHI





HOTUBA YA KATIBU TAWALA MKOA NDUGU FAISALI  ISSA WAKATI WA UZINDUZI WA KITUO CHA PAMOJA CHA KUTOA HUDUMA KWA WAATHIRIKA WA UKATILI WA KIJINSIA. IMESOMWA KWA NIABA YAKE NA MHANDISI WA MAJI MKOA WA KILIMANJARO ALFRED SHAYO.


Ndugu Mkuu wa Wilaya ya Hai , Novatusa Makunga
Mh Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya hai,Clement Kwayu
Ndugu mwakilishi wa UNICEF Tanzania
Ndugu mwakilishi wa  Serve the Children Tanzania
Ndugu Mwakilishi wa Kamishna- Polisi
Ndugu Mkurugenzi wa Watoto-Wizara ya Maendeleo ya Jamii
Ndugu Wawakilishi wa asasi za kiraia,Madhehebu na Dini
Viongozi wote ,mabibi na mabwana

Awali ya yote nimefarijika kupata nafasi hii muhimu ya kushuhudia uzinduzi wa kituo cha pamoja cha kutolea huduma kwa waathirika wa Ukatili wa kijinsia hasa watoto.
Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa kituo hiki utakuwa chachu ya kutolewa kwa taarifa za ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto baada ya upatikanaji wa huduma hizo kurahisishwa.
Ndugu wananchi, kituo hiki kimezinduliwa siku ambayo pia ni siku ya kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika huku kauli mbiu ikiwa ni ”KUPATA ELIMU BORA NA ISIYO NA VIKWAZO NI HAKI YA KILA MTOTO.”   kutokana na kauli mbiu hii ni vema kila mmoja wetu kwa kutumia nafasi aliyo nayo atimize wajibu wake ili kuhakikisha mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu bora.
Tumieni fursa iliyopatikana ya kituo cha pamoja kwa ajli ya kutoa taarifa za ukatili kwa watoto,ukatili ambao wakati mwingine unamsababishia mtoto kukosa fursa ya Elimu.
Acheni tabia ya kumaliza masuala ya ukatili wa kijinsia katika  ngazi ya familia kwakufanya hivyo kamwe hamtaweza kutokomeza matukio haya.
Tunajua kuwa wakati mwingine inakuwa ni vigumu kwa wanandugu kufikishana katika vyombo vya sheria ili kutovunja undugu, lakini tukiendelea kuwafumbua macho hawa watu eti kwasababu ni ndugu matukio kama haya yataisha, sasa je mtoto atapata haki yake ya msingi na kutimiza kauli mbiu ya mwaka huu?
Ni wakati wa mabadiliko na mabadiliko yanaanzia Katika Wilaya ya Hai kwakutumia vema rasilimali zilizopo ambazo ni pamoja na Kituo Jumuishi cha pamoja.

Mkuu wa Wilaya  na pamoja na  timu yako ya Wataalam,
Napenda kuwapongeza kwa mafanikio mliyofikia baada kuanzisha mfumo wa ulinzi kwa mtoto na sasa kufikia hatua ya kuwa na kituo hiki.Ni mafanikio ambayo jamii ya wanahai lazima wajivunie.Naamini wakati  umefika kwa Wilaya zingine kuja kujifunza kutoka kwenu kwa mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzisha mfumo wa ulinzi kwa mtoto
Katika taarifa zenu awali mmesema mmefanikiwa kupunguza makao ya watoto kutoka 22 hadi 7, tumieni ujuzi na mbinu mlizo tumia kupunguza makao hayo kusaidia Wilaya za jirani ambazo bado makao ya watoto yanaonekana kama suluhu ya kusaidia watoto walio katika mazingira hatarishi huku baadhi ya wenye makao hayo wakitumia kama njia ya kujinufaisha.
Ni wazi kuwa kuongezeka kuripotiwa kwa matukio ya watoto waliofanyiwa ukatili na watu wazima waliofanyiwa ukatili wa kijinsia  umesababisha na elimu mliyoitoa katika jamii ni vema mkaendelea kutoa elimu hiyo hasa kwakutumia vyombo vya habari.

Kufunguliwa kwa kituo hiki iendeleze  ushirikiano uliopo kati ya ofisi ya ustawi wa jamii ,dawati la  na watoto jinsia,mahakama ,elimu, na hospitali, kuwahudumia watoto na wadau wengine

Ndugu wananchi,
Serikali yetu inatoa shukrani kwa wafadhili waliosaidina katika kufanikisha ujenzi wa kituo hiki ambao ni UNICEF Tanzania na Save the children Tanzania. Fedha zilizotumika katika ujenzi wa kituo hiki naamini hazijapotea bali zitaleta matunda mazuri. Tunaomba muendele kuisaidia serikali katika kufikisha huduma kwa jamii. Serikali inatambua mchango wenu, na inaahidi kusimamia vema michango yoyote ile mtakayoitoa.
Natoa wito wito kwa wazazi,walezi na wadau wengine pamoja na viongozi wa ngazi zote kuendelea kutoa taarifa  za ukatili dhidi ya watoto na ukatili mwingine wa kijinsia ili kuweza kuwa na Jamii ilivyostawi na kuwa na maendeleao katika nchi.



No comments:

Post a Comment