Monday, May 19, 2014

WATAALAM WA AFYA WATOA TAADHARI YA UGONJWA WA DENGUE KWA WAKAZI WA WILAYA YA HAI




WANANCHI wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wametahadharishwa kuwa makini  na kujikinga na mbu  anayeeneza ugonjwa wa dengue kutokana na Wilaya hiyo kuwa na viashiria vya  ugonjwa huo .

Tahadhari hiyo imetolewa na Madaktari  kutoka Hospitali ya  Wilaya ya Hai  kufuatia kuwepo na taarifa ya  watu wawili  wenye  viashiria vya ugonjwa huo ambao umekuwa tishio kwa wananchi wengi tangu uliposhika kasi ukianzia jijini Dar Es Salaam. 

Wakizungumza  katika Kituo cha Redio Boma Hai FM   madaktari wa Hospitali ya Wilaya hiyo Dkt Julias Massawe  na Happynes Ndenshau walisema mpaka sasa kuna viashiria vya ugonjwa huo kuwepo Wilaya hapa kutokana na watu  wawili kusadikiwa kuwa na viashiria vya  ugonjwa huo 

Dkt Massawe alisema  watu hao wawili ambao  mmoja anasadikiwa kuwa alitokea jijini Dar Es  Salaamu ambaye  ni mkazi wa kijiji cha Narumu na mwingnine   ni  alitokea Arusha  ambaye ni mkazi wa mtaa wa Kibaoni na kwamba vipimo vyao vimepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Alisema kutokana na watu hao kuwa na viashiria vya  ugonjwa wa Dengue na kulazwa katika Hospiali ya St Jose ya mjini Moshi kufuatia hali hiyo Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari mapema pindi wanapohisi kuwa na dalili za  ugonjwa huo kwa kufika katika kituo cha afya kilichopo karibu  ili waweze kupatiwa huduma.

Nae Dkt Ndenshau alisema hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni  kutoa elimu kwa wataalam wa afya waliopo katika vituo vyote vya afya ili wanapobaini mtu mwenye dalili ili wanapoona mtu mwenye dalili hizo hatua zichukuilwe mapema ikiwa ni pamoja kupeleka vipimo vyake katika Hospitali ya Wilaya kwa hatua zingine zaidi.

Hatua zingine zilizochukuliwa na Uongozi wa Hospitali hiyo ni pamoja nakutoa elimu kwakutumia  njia mbali mbali ikiwa ni pamoja na kituo cha Redio Boma Hai FM, matangazo ya barabarani kwa kuwasisitiza wananchi juu ya usafi wa mazingira hasa kukata majani ,kutoacha madimbwi ya maji lakini pia kupiga dawa kwenye  maeneo yenye miti mingi na hasa kwa wale ambao wamelima karibu na nyumba zao.

Alisema kwa sasa hakuna tiba wala chanjo ya ugonjwa huo, hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya maambukuzi  ya magonjwa yanayosababishwa na mbu.

“mbu  wanaoeneza Dengue ni Aides na si anofelis kama jinsi baadhi watu wanavyosema kwani mbu huyo hueneza  malaria,mbu hawa ung’ata mchana hivyo ni vema wananchi wakachukua tahadhari kwa kuvaa nguo ndefu,kwa wanao lala mchana walale kwenye neti na kuteketeza mazalia ya mbu’alisema Dk. Ndenshau.

Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuumwa kichwa hasa sehemu ya mebele karibu na macho,kichefuchefu,kutokwa na upele mdogomdogo mwilini ,kutokwa na damu sehemu za wazi za mwili.

Kuhusu Madaktari hao wamewataka wananchi kufika katika kituo chochote cha afya kwa ajili ya vipimo mara tu watakapohisi dalili kama walizozitaja kwa ajili ya kupata huduma na kuwatoa hofu wananchi wasio kuwa na uwezo wa kulipia gharama za matibabu kuwa vipimo vya ugonjwa huo vinagharamiwa na serikali kwa watakao gundulika wana dalili za ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment