Tuesday, April 29, 2014

WANANCHI WAOMBWA KUCHANGIA DAMU



Wananchi wa Wilaya ya Hai  wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uchangiaji wa damu salama ili kunusuru vifo vingi vya wanawake baada ya kujifungua vinavyotokana na upotevu wa damu nyingi na kukosekana kwa damu.

Uchangiaji huo unatarajia kufanyika Leo  katika shule ya Sekondari Hai kuanzia saa tatu kamili.
Mratibu wa chama cha msalaba mwekundu, kisaidizi cha serikali (Red cross) wilaya ya Moshi David Sinda aliyasema hayo wakati akizungumza na Redio Boma Hai  kuhusiana na suala la uchangiaji wa damu salama kwa hiari.

Sinda alisema uhaba wa damu katika benki ya damu imekuwa chanzo cha wanawake wengi kupoteza maisha baada ya kujifungua kutokana na kutokwa na damu nyingi huku wananchi wengi hawana utayari wa kuchangia damu.

“Tuwasaidie hawa wanawake wanaopoteza maisha baada ya kujifungua kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchangiaji wa damu salama kwa hiari ambalo linaloendelea hivi sasa”alisema Sinda

Kwa upande wake mratibu wa huduma za kutunza wagonjwa majumbani mkoa wa Kilimanjaro Leticia Mwigamba alisema kuna uhitaji mkubwa wa damu kwa wanawake, wazee na watoto ambao wameonekana kuathirika zaidi.

Akizungumzia suala la baadhi ya watumishi kutokuwa waaminifu na kuwauzia damu watu wenye uhitaji wa damu Mwigamba alisema ni vyema wananchi wakatoa taarifa sehemu husika ili hatua zichukuliwe kukomesha hali hiyo.

“Kuna baadhi ya wauguzi sio waaminifu wanawauzia damu wagonjwa tunatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa sababu huduma ya damu ni bure kwa wagonjwa hospitalini” alisema “Leo tunaendesha zoezi la uchangiaji wa damu salama hapa wilayani Hai ikiwa ni katika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya chama cha msalaba mwekundu ulimwenguni ambayo huadhimishwa kila tarehe 8 may, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni” my red cross story” na kitaifa itafanyika Jijini Mbeya” Alisema Mwigamba

No comments:

Post a Comment