Friday, April 6, 2018

Wananchi Watakiwa Kutunza Miti Wanayootesha


Mkuu wa Wilaya ya Hai, Onesmo Buswelu akipanda mti kuashiria uzinduzi wa wiki ya kupanda miti uliofanyika Kijiji cha Mtakuja tarehe 05 Aprili 2018.
(Picha zote na Adrian Lyapembile)

Na Hellen Shayo
HAI

MKUU wa wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Onesmo Buswelu amewataka wananchi kutunza miti inayooteshwa katika kipindi hiki cha mvua ili iweze kukua na kukabiliana na hali ya ukame kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya upandaji  miti ambayo kiwilaya ilifanyika kijiji cha Mtakuja kata ya Kia, Buswelu amesema kuwa zoezi la kupanda miti limekuwa likifanywa kila mara la jamii imekuwa ikipanda kwa ajili ya maadhimisho na kusahau jukumu la kuitunza.


Amesema kuwa kutokana na wananchi kupanda miti pasipo kuitunza kunafanya nchi kuendelea kuwa jangwa hali ambayo imesababisha hata vyanzo vya maji kukauka na kuepelekea kuwepo kwa mgawo wa maji.


Amewaagiza viongozi wa kijiji cha Mtakuja pamoja na kampuni ya KADCO kuhakikisha  kuwa miti iliyooteshwa inatunzwa na kuhakikisha kuwa haikatwi hovyo, na kwambi hatua kali zitachukuliwa kwa  yeyote atakaye kata miti hovyo pasipo kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.


Amefafanua kuwa  Wilaya hiyo  imebahatika kuwa kitovu cha utalii kutokana na kuwa karibu na  Mlima Kilimanjaro ili kuonesha mfano kwa wageni watokao watokao nje ya Nchi, waone Tanzania yenye kujali swala zima la Mazingira.

Awali akisoma risala kwa niaba ya Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Albert Mwakipesile  amesema kuwa katika uzinduzi huo  wanatarajia kupanda miti elfu moja na mia tano, na kwa mwaka huu wanalo lengo la kupanda miche ya aina mbalimbali za miti ipatayo  milioni moja na nusu kwa kipindi cha  mvua za masika.


Naye mwenyekiti wa kijiji cha mtakuja, Tehera Moleli ameahidi kuwa atajitahidi kuhamasisha wananchi, kutumia sheria na kuwaelimisha wananchi juu ya faida za Upandaji miti na kuhakikisha zoezi hilo linazingatiwa na kufanikiwa katika kijiji chake.

Kwa upande wake Afisa Maliasili Wilaya ya Hai, Mbayani Mollel amewakumbusha viongozi wa vijiji kitunza na kuilinda miti iliyooteshwa katika kipindi cha mvua ili kuendelea kutunza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye huku akiahidi kuwapa ushirikiano pale watakapohitaji msaada wa kitaalamu katika utunzaji wa mazingira.

No comments:

Post a Comment