Saturday, April 28, 2018

DC Aagiza Mto Sanya Usafishwe Kudhibiti Mafuriko


Mkuu wa Wilaya ya Hai Onesmo Buswelu (aliyevaa suti) akitoa maagizo kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya kushirikiana na wananchi kurekebisha miundombinu ya Mto Sanya wakati wa ziara yake ya kukagua madhara yaliyosababishwa na mafuriko katika Kijiji cha Sanya Station mapema Aprili 19, 2018. (Picha na Davis Minja)


Na. Adrian Lyapembile
HAI

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Mhe. Onesmo Buswelu amewaagiza wataalamu wa mazingira, kilimo na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kushirikiana kufanya usafi ndani ya mto Sanya eneo la Sanya Staion kuondoa mlundikano wa mchanga kwenye kina cha mto huo pamoja na kupanda miti na makingamaji kwenye eneo la mto alipofanya ziara ya kukagua madhara yaliyosababishwa mvua zinazoendelea kunyesha na kufanya mto kuacha njia ya asili na kuanzisha mkondo mwingine.

Buswelu ametoa maagizo hayo leo tarehe 19 April 2018 alipofika eneo la ardhi lililoharibiwa na maji ambayo yameanzisha mto mwingine unaoelekea kwenye mashamba na makazi ya wananchi wa kijiji cha Sanya Station katika kata ya Kia na kusababisha uharibufu wa mazao.
Mkuu wa Wilaya pia ameliagiza jeshi la Mgambo wilaya ya Hai kushirikiana na wananchi katika kutoa nguvu kazi wakati wa zoezi la kusafisha mto huo kwa lengo la kukamilisha kazi hiyo kwa haraka ili kuzuia uharibifu mwingine unaoweza kutokea kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.


Pamoja na agizo hilo, Buswelu amewataka wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mto huo kuchukua hatua za kutunza mazingira kwa kuotesha miti na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo ndani ya mita 60 kutoka eneo la mto.


Akizungumzia uharibifu uliojitokeza kwenye mazao ya wakulima, kaimu mtendaji wa kata ya Kia Simba Lema amesema zaidi ya ekari 477 zimepitiwa na maji na kwamba tathmini inaendelea kufanywa ili  kubaini gharama halisi ya madhara yaliyopatikana kwenye mazao.


Naye meneja wa TARURA wilaya ya Hai mhandisi Charles Marwa amesema kutokana na umuhimu wa mto huo kwa jamii watasimamia zoezi hilo kwa kutoa ushauri wa kitaalam na kwa haraka zaidi kama walivyoagizwa na Mkuu wa wilaya  ili kuwawezesha wananchi walioathiriwa na kuchepuka kwa mto huo kuendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi.


No comments:

Post a Comment