Friday, November 10, 2017

WATUMISHI WATORO KUWAJIBISHWA KINIDHAMU

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Ndugu Yohana Elia Sintoo akizungumza na watumishi wa Halmashauri yake walioripoti vituo vya kazi wakitoka masomoni. (Picha na Riziki Lesuya)

Na. Adrian Lyapembile
HAI

Tabia ya kuchelewa kuripoti vituo vya kazi kwa watumishi wa umma wanaopewa ruhusa kwenda masomoni imekemewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo.


Akizungumza kwenye kikao maalumu alichofanya na watumishi wa halmashauri hiyo mapema leo, Sintoo amesema tabia hiyo haivumiliki na inapingana na miongozo ya utumishi wa umma inayoelekeza mtumishi kufika kituo cha kazi mara baada ya kumaliza masomo yake.

Sintoo ameongeza kuwa iwapo kutakuwa na mambo ambayo mtumishi hajayakamilisha ni vema akaripoti kituo cha kazi na kuomba ruhusa ya kwenda kukamilisha mambo yake kuliko kuendelea na mambo binafsi wakati jamii inamsubiri kupata huduma yake.

“Nakuagiza Afisa Utumishi kufuatilia wale wote waliokuwa masomoni waliotakiwa kuwa wamesharipoti vituo vya kazi lakini bado wanafanya mambo binafsi; shikilia mshahara na hatua stahiki za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao”. Aliongeza Sintoo.

Aidha Sintoo amezungumzia mpango wa halmashauri yake kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kufunga vifaa vya kielektroniki vitakavyosimamia utaratibu wa watumishi kuingia na kutoka kazini na kuachana na kutumia madaftari ya mahudhurio ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kutumika kutoa taarifa zisizo za ukweli.

Ameagiza halmashauri kuanza mara moja mchakato wa kutafuta na kufunga vifaa hivyo ili kupunguza matumizi mabaya ya muda na kuongeza ufanisi miongoni mwa watumishi.

Aidha Sintoo amewakumbusha watumishi wote katika Halmashauri ya Hai kufanya kazi kwa bidii kwa kuwahudumia wananchi bila ubaguzi lakini zaidi kutumia vizuri muda wa kazi kwa kutekeleza majukumu.









No comments:

Post a Comment