Monday, November 6, 2017

MKURUGENZI HAI AHIMIZA WATUMISHI KUTUMIA SACCOSS KUJIENDELEZA KIUCHUMI


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Ndugu Yohana Elia Sintoo (Picha kutoka Maktaba)


Na. Adrian Lyapembile
HAI


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai  Yohana Elia Sintoo amewataka wafanyakazi wa Umma katika Wilaya za Hai na Siha kushirikiana kwa kutumia vyama vya ushirika kwani ndiyo suluhisho halisi la maswala ya kiuchumi.

Sintoo ameyasema hayo wakati akitoa salamu za Halmashauri yake kwenye Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Hai Rural Teachers Saccoss uliofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya Chuo cha Ufundi Hai.

Amewataka watumishi kutumia vizuri huduma za saccos kwani zinasaidia katika kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu na kuwataka kuacha kutumia vyama ambavyo havijasajiliwa ili kuepuka usumbufu.

Pia amebainisha wazi kuwa Halmashauri yake ipo tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika na kuwataka watumishi wote wawe mabalozi wa kuwashawishi watumishi wenzao ambao bado hawajajiunga na saccoss kujiunga ili kuiongezea nguvu Hai Rural Teachers Saccoss.


Naye Meneja wa HRT Saccoss Upendo Lyatuu ameeleza kuwa chama hicho kilianza mwaka 2000 idadi ya wanachama waanzilishi wakiwa 67 kikiwa na mtaji wa Tshs. 335,000/= na hadi kufikia Septemba 2017 chama kimefikisha wanachama 2365 na mtaji wa Tshs. 6,064,652,078/= na kwamba tangu chama hadi kufikia Septemba 30, 2017 jumla ya Tshs. 24,031,015,000/= zimetolewa kama mikopo kwa wanachama. 





No comments:

Post a Comment