Monday, November 6, 2017

NAIBU KATIBU MKUU APONGEZA USTAWI WA JAMII WILAYA YA HAI


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ndugu Hassan Khatib Hassan (Waliokaa aliyevaa Suti) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa timu ya Ulinzi wa Mtoto Wilaya ya Hai alipotembelea Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Polisi Wilaya ya Hai. (Picha na Edwin Lamtey)



Na Adrian Lyapembile
HAI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ndugu Hassan Khatib Hassan ametoa pongezi kwa kitengo cha Ustawi wa Jamii Wilaya ya Hai kwa utendaji mzuri na utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo swala la ulinzi wa mtoto.


Ndugu Hassan Khatib Hassan akiambatana na timu ya wataalamu kutoka wizara yake amesema hayo wakati wa ziara ya mafunzo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Hai yenye lengo la kujionea na kujifunza namna kitengo cha Ustawi wa Jamii kinavyofanya kazi.

Amesema wamefurahishwa na ushirikiano waliouona kati ya wataalamu wa Halmashauri na watendaji katika ngazi zote hadi kwenye ngazi ya kijiji pamoja na ushirikiano mzuri na dawati la jinsia na watoto la Polisi Wilaya ya Hai ambapo wamejionea namna kazi zinavyotekelezwa kwa kushirikiana na kwenda pamoja hatua kwa hatua huku kila kundi likitekeleza majukumu yanayowahusu.

Aidha Ndugu Hassan Khatib Hassan ameonesha kufurahia suala la uhamasishaji na elimu dhidi ya ukatili inavyotolewa kwa jamii ambapo wameshuhudia elimu ikitolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara ya vijiji, kutembelea kwenye shule pamoja na kutumia vyombo vya habari.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Hai; Helga Simon amesema wamefarijika sana kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa kuja kujifunza wanavyotekeleza majukumu yao kwani imewaongezea ari ya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Katika ziara hiyo, timu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikujumuisha Mkurugenzi wa Idara ya Wanawake na watoto, Maafisa Ustawi wa jamii wa kitaifa na wilaya wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Hassan Khatib Hassan walitembelea ofisi za Ustawi wa Jamii Wilaya, One Stop Centre iliyopo Hospitali ya Wilaya, Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Polisi Wilaya pamoja na kijiji cha Romu kilichopo kata ya Masama Mashariki kujionea jinsi timu za ulinzi wa mtoto zinavyofanya kazi.

Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Hai Helga Simon (aliyesimama) akitoa maelezo ya namna Kitengo cha Ustawi wa Jamii kinavyofanya kazi kwa ugeni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Ndugu Hassan Khatibu Hassan. (Picha na Edwin Lamtey)


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mhandisi Nyakaraita Mwita akiwakaribisha wageni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Ndugu Hassan Khatibu Hassan. (Picha na Edwin Lamtey)


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Zanzibar Ndugu Hassan Khatibu Hassan (wa pili kutoka kulia waliochuchumaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Timu ya Ulinzi wa Mtoto ya Kijiji cha Romu Kata ya Masama Mashariki. (Picha na Edwin Lamtey)


No comments:

Post a Comment