Wednesday, October 11, 2017

WAFUGAJI WANOLEWA KUONGEZA UPATIKANAJI MAZIWA


Na. Riziki Lesuya  
HAI

Meneja mradi wa maziwa kutoka Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) Thom Olesika akizungumza na washiriki wa mafunzo kwa wafugaji (hawapo pichani)

Wafugaji  katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuthamini na kutunza miradi ya maendeleo inayoanzishwa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili miradi hiyo iweze kudumu na kuleta tija kwa jamii kama ilivyokusudiwa.

Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo  wafugaji wa mfano yaliyofanyika  Wilayani Hai,  meneja mradi wa maziwa kutoka shirika la maendeleo la Uholanzi (SNV) Thom Olesika amewataka wafugaji hao  kutambulisha mradi huo kama wa kikundi ili kuwawezesha wananchi kuwa na umiliki wa mradi kitu ambacho kitasaidia mradi kuwa endelevu.
Mafunzo ya ufugaji bora wenye kuongeza kiwango cha maziwa yameshirikisha vikundi 22  vinavyojishughulisha na ufugaji  wa ng’ombe na uuzaji wa maziwa katika wilaya ya Hai.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Hai; Elia Machange amelishukuru shirika la SNV kwa kusaidia kufanikisha mafunzo hayo ambayo na kuwataka wafugaji waliohudhuria kutumia elimu waliyoipata kwa kuwaelimisha wafugaji wenzao ili kuimarisha ufugaji bora na kuinua kiwango cha upatikanaji maziwa.  
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo baadhi ya washiriki wameishukuru SNV kwa hatua hiyo huku wakiahidi kufanyia kazi mafunzo waliyoyapata kwa kuwa mfano wa kuigwa na wafugaji wenzao.
Bi Faith Lema kutoka kikundi cha wamando kijiji cha Nkuu amewaomba wawezeshaji wa mafunzo hayo waendelee kutoa mafunzo ya mara kwa mara  ili wafugaji wengi waweze kunufaika na ufugaji huku Erick Urrasa akisema wanatarajia ubora wa maziwa utaongezeka pamoja na ng’ombe bora ambao watasaidia kuinua mitaji yao.

Mradi huo wa kuimarisha ufugaji na kuongeza uzalishaji wa maziwa katika wilaya ya Hai unafadhiliwa na shirika la maendeleo la Uholanzi (SNV) ukiwa na lengo kuu la kuinua uchumi wa wafugaji hasa wanawake na vijana na kuongeza upatikanaji wa maziwa kwa wakazi wa wilaya ya Hai na maeneo ya jirani.
Baadhi ya Wafugaji wakifuatilia mada kwenye mafunzo ya kuboresha ufugaji na kuongeza upatikanaji wa maziwa.




No comments:

Post a Comment