Wednesday, October 11, 2017

MATUMIZI YA MFUMO WA KIELEKTRONIKI KUONDOA CHANGAMOTO HUDUMA ZA AFYA

Na. Latifa Botto  
HAI

Matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kutolea huduma za afya (GOT HOMIS)  ulioboreshwa utasaidia juhudi za kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo mahospitalini ikiwa ni pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo  (aliyevaa suti) akiwa na washiriki wa mafunzo ya mfumo ya kielektroniki wa huduma za afya.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hamashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya kuwaongezea ujuzi wataalamu katika halmashauri zote za Mkoa wa Kilimanjaro wakiwemo madaktari, wafamasia,wataalamu wa Tehama na watumishi wengine wanaohusika katika kuhudumia wagonjwa.

Amesema kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo katika hospitali, serikali imeona ni vema kutumia mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato ili kudhibiti upotevu wa mapato kitu kinachoonekana kuwa kiini cha changamoto mbalimbali zilizopo kwa sasa.

Sintoo ameongeza kwa kusema kuwa mfumo huo umejikita zaidi katika kudhibiti mapato bila kuwa na upotevu na kwamba mfumo huo utaanza kutumika hivi karibuni.

Wakati huo huo; Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dkt. Irine Haule  amewaasa watumishi wa afya kukubali mabadiliko kwa kujifunza na kuelewa vizuri namna ya kutumia mfumo huo ulioboreshwa ili kufanikisha lengo la serikali la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwani upatikanaji mzuri wa mapato unapelekea kupata huduma bora zaidi hospitalini.


Mfumo wa kielekroniki wa kutolea huduma za afya ni moja ya mifumo inayotekelezwa na serikali katika kuboresha huduma zinazotolewa kwa mwananchi na kwamba kuanza kutumika kwa mfumo huo kutadhibiti upotevu wa mapato hivyo kuimarisha uwezo wa hospitali katika kila ngazi ya huduma kuweza kujihudumia kutokana na mapato yanayokusanywa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai;
Yohana Sintoo akisisitiza jambo wakati wa kufungua
mafunzo ya siku tatu ya mfumo wa  kielektroniki
kwa wataalamu wa afya.

1 comment: