Wednesday, August 2, 2017

MKURUGENZI WA WILAYA YA HAI AWATAKA WANAWAKE KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI

Baadhi ya wanawake waliohudhuria Uzinduzi wa Baraza la Kuwezasha Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Hai, wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi. 


HAI - KILIMANJARO

WANAWAKE wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za kiuchumi zinapojitokeza kwani maendeleo yaangalii jinsia ya mtu bali namna mtu anavyojituma na kujishughulisha.


Hayo yamesemwa leo mjini Bomang’ombe na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwenye hotuba iliyosomwa kwa niamba yake na Edward Ntakiliho kwenye tukio maalumu la kuzindua Baraza la kuwezesha wanawake Kiuchumi ambapo Wanawake toka vikundi mbalimbali vya uwekezaji na ujasiriamali walikutana.

Amesema kuwa kwa muda mrefu Wanawake wamekuwa hawapati fursa za kutosha za kiuchumi kutokana na kukosekana kwa usawa katika fursa,uwezo na kupata mitaji ajira na baadhi ya malipo ya kazi kwa wanawake yamekuwa siyo sawa na Wanaume.

Ntakiliho ameongeza kuwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wa Wananchi kiuchumi limepewa dhamana ya kusimamia Sera na utekelezaji wa Sera ya Taifa kwa kuwaongoza Wananchi katika kufanikiwa kiuchumi kupitia Halmashauri za Wilaya na Taasisi nyingine.

Ameongeza kuwa Jukwaa la Wanawake litaweza kuongeza uelewa wa wanawake katika masuala ya kiuchumi, biashara na upatikanaji wa mitaji na njia sahihi ya kutegemeana kiuchumi kwa halmashuri ya wilaya kuhakikisha kuwa inasimamia majukwaa ya kiuchumi katika kata na kufanya mikutano kila baada ya miezi sita ndani ya wilaya.

Kwa upande wake Mratibu wa Jukwaa la Wanawake  Wilaya Frank Urio amesema kuwa jukwaa hilo litaweza kuwakutanisha  wanawake katika biashara na ujasiriamali  wa bidhaa mbalimbalil ikiwemo ubunifu wa kuweza kumiliki viwanda kama sera ya Nchi inavyoelekeza.

Amesema kuwa Wanawake wamekuwa wakichangia pato la Familia mpaka pato la Taifa kwa utashi walio nao katika kuwekeza katika vikundi mbalimbali na kuweza kuji kwamua kiuchumi hivyo kuwa  nguzo muhimu ndani ya Familia na jamii.

Uzinduzi wa Baraza la Kuwezesha Wanawake Kiuchumi ni utekelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasan yanayoelekeza kila Wilaya na Mkoa  kuunda na kuendesha majukwaa ya Wanawake kwa lengo la kuwakutanisha wanawake kujadiliana fursa, changamoto na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa kaya na hatimaye wa Taifa ambapo wanawake wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wamekuja na kauli mbiu isemayo  “WANAWAKE WAKIUNGANA WANAWEZA”.


1 comment:

  1. Hellow tanzania kuna kampuni imefunguliwa maeneo ya rau msamaria karibu na car inajishuhulisha na uuzaji wa malighafi kwa ajili ya kutengenezea sabuni,shampoo, pamoja na jik,wote mlio ndani ya mkoa wa kilimanjaro karibuni tunawakaribisha
    kwa mawasiliano zaidi naomba tuwasiliane kupitia no 0747665695 au 0743782384

    ReplyDelete