Thursday, March 27, 2014

WANANCHI 8,786 KUPATA HUDUMA YA MAJI SAFI NA SALAMA

Jumla ya wananchi 8,786 wa vijiji vya Sanya Station, Mtakuja, Tindigani na Chemka Wilayani Hai wanatarajia kupata huduma ya maji safi na salama baada ya kukamilika kwa upanuzi wa mradi wa maji wa Losaa-KIA unaotarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.33.



Akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Mradi huo mbeye Timu ya Ufuatiliaji ya Mkoa iliyomwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa ,Mhandisi wa maji WIlaya Mwita Nyakaraita kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wialaya ya Hai, alisema mradi huo umegawanywa katika mafungu (lots) nne za ujenzi ili kurahisisha kazi ya ujenzi kwa lengo la kuwapatia wananchi wa vijiji hivyo huduma hiyo muhimu kabla ya tarehe 30/06/2014.

Alisema kazi zitakazofanywa na wakandarasi ni pamoja na kuchimba mtaro na kulaza bomba katika umbali wa mita 64,131,ukarabati wa matanki matatu,ujenzi wa matanki mapya mawili ya juu(raiser tanks) yenye ujazo wa lita 30,000 kila moja na ujenzi wa vilula 37.

 Nyakaraita alisema katika fungu la kwanza mradi huo unaoanzia katika tanki la vunja msukumo(PRT) la Mungo wa Mae hadi tanki la vunja msukumo la Somali Settlement na unatarajia kutumia kiasi cha shilingi 1,119,500,000 na kazi hiyo inafanywa na mkandarasi M/S Deniko ,fungu la pili likianzia katika tanki la Vunja Msukumo (PRT) la Somali Settlement kupitia tanki la Mlima Shabaha hadi kijiji cha Tindigani na unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi 899,864,000 na unatekelezwa na mkandarasi M/S Progress Investments Co.Ltd akishirikiana Nure Building & Civil Contractors Co.Ltd.

 Katika taarifa hiyo pia imeonyesha kuwa fungu la tatu linaanzia katika kijiji cha Tindigani hadi kijiji cha Chemka ambao unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi 622,032,550 ambao utatekelezwa na mkandarasi M/S Mbesso construction Co.Ltd huku fungu la nne ambalo linagharimu kiasi cha shilingi 705,295,248 unaanzia katika kijiji cha Tindigani hadi Kijiji cha Mtakuja na unatekelezwa na mkandarasi Motosach Construction Ltd.

Aidha alisema Halmashauri inakabiliana na changamoto mbali mbali katika kutekeleza mradi huo ikiwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kulalamika kuharibiwa mazao yao kutokana namsimu wa kilimo unaoendelea ambapo jitihada za kutoa elimu zinafanyika ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwa upande wake Mhandisi wa Mkoa amewaagiza wa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuhakikisha kuwa wananunua vifaa ambavyo vina viwango vinavyostahili ili kuiepusha serikali kupata hasara inayoweza kuzuilika na kuhakikisha kuwa vifaa vinavyotumika vinatunzwa ipasavyo ili kuepusha vifaa hivyo kupunguza kiwango chake kabla ya kuanza kutumika akitolea mfano utunzaji wa mabomba ya plastiki ambayo yanapaswa kuhifadhiwa katika eneo lenye kivuli na lisililo na joto kali.

No comments:

Post a Comment