Wednesday, January 3, 2018

HAI YAPONGEZWA KWA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA AFYA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akikagua miradi ya maendeleo katika hospitali ya wilaya ya Hai alipofanya ziara ya kikazi. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wilaya ya Hai Yohana Sintoo. (Picha na Omary Mlekwa)


Na. Adrian Lyapembile
HAI


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jaffo ameipongeza halmashauri ya wilaya ya hai kwa kuendelea kuboresha miundombinu katika hospitali ya wilaya hiyo itakayofanikisha kutekeleza azma ya serikali kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake.


Mhe. Jaffo ameyasema hayo kwenye ziara yake ya kikazi katika wilaya ya Hai ambapo ametembelea hospitali ya wilaya hiyo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa wodi ya magonjwa mchanganyiko, ununuzi wa jenereta la kisasa la kufua umeme pamoja na ujenzi wa duka la dawa.

Amesema hatua iliyofikiwa ni nzuri kwenye ujenzi wa jengo la wagonjwa mchanganyiko na duka la dawa huku akiongeza kuwa uwepo wa duka la dawa la kuaminika katika wilaya ni jambo jema ambalo litasaidia wananchi wa wilaya ya Hai na maeneo jirani kupata dawa kwa uhakika.

Mapema akitoa maelezo ya ujenzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai Yohana Sintoo amemwambia waziri Jaffo kuwa ujenzi wa duka la dawa umekamilika na kwamba kinachofanyika kwa sasa ni kuweka samani pamoja na kufunga vifaa vinavyohitajika.


Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Irene Haule amesema pamoja na kuwa jengo hilo limejengwa maalumu kwa ajili ya wanachama wa bima za afya lakini litatumika kama kitega uchumu kwa hospitali hiyo ambapo litatoa huduma kwa wagonjwa wengine wasio wanachama wa bima ambao watanunua dawa lengo kuu likiwa ni kuondoa tatizo la kukosekana dawa kwenye hospitali ya wilaya na maeneo ya jirani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo akitoa maelezo ya jenereta la kisasa la kufua umeme lililonunuliwa kwa matumizi ya Hospitali ya wilaya ya Hai mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Yohana Sintoo akitoa maelezo ya jengo la wodi ya magonjwa mchanganyiko linalojengwa kwenye Hospitali ya wilaya ya Hai mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo (hayupo pichani).


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Hai alipofanya ziara ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya (picha zote na Omary Mlekwa). 



No comments:

Post a Comment