Friday, May 18, 2018

Watumiaji wa Barabara Watakiwa Kutii Sheria za Usalama

Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sauda Mohamed akizungumza na wananchi kwenye Kipindi cha Siku Mpya kinachurushwa na Redio Boma Hai 89.3 FM. 
(Picha na Adrian Lyapembile)

Na Gasper Mushi
HAI
Wito umetolewa kwa wapanda pikipiki mkoa wa Kilimanjaro kuvaa kofia ngumu (Helmet) wanapotumia vyombo hivyo vya moto ili kujilinda na kufuata sheria za usalama barabarani.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sauda Mohamed wakati akizungumza na wananchi wa moka huo kupitia Redio Boma Hai FM katika kipindi cha Siku Mpya kinachoruka kila siku saa 11 alfajiri hadi saa 3 kamili asubuhi.

Kamanda huyo wa usalama barabarani amesema kuwa kutakuwa na oparesheni maalumu katika wilaya ya Hai ya kuwakamata waendesha pikipiki wote wasiovaa kofia ngumu na kuwachukulia hatua za kisheria.

Kamanda Sauda amesisitiza kuwa kila mwendesha pikipiki anatakiwa kufuata sheria zote za usalama barabarani kama watumiaji wengine wa vyombo vya moto na kuongeza kuwa ni makosa kwa mwendesha pikipiki kukipita chombo kingine cha moto (kuovateki) kwa upande wa kushoto na kwamba atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake Mkuu wa Usalama barabarani Wilaya ya Hai ASP Abdalah Mbaruku amesema kuwa oparesheni hiyo itaanza wiki hii na itakuwa endelevu kuhakikisha kuwa kila mtu anatii sheria bila shuruti kwa kuvaa kofia ngumu na kufuata sheria za usalama barabarani kwa ajili ya usalama wa mali na maisha ya watumia barabara wote.
Mkuu wa Kitengo cha Usalama barabarani Mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sauda Mohamed akiwa na  Mkuu wa Usalama barabarani Wilaya ya Hai ASP Abdalah Mbaruku wakitoa elimu ya usalama barabarani kwa wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya jirani kwa kupitia Redio Boma Hai 

Mbaruku ameongeza kuwa kosa la kushindwa kuvaa kofia ngumu linawahusu madereva wa pikipiki pamoja na abira wao na kwamba abiria atawajibishwa kwa kutovaa kofia na dereva atakayeshindwa kumpatia abiria wake kofia ngumu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwani kila mpanda pikipiki awe dereva au abiria anao wajibu wa kuvaa kofia ngumu.

Aidha watumiaji wote wa barabara wameaswa kujielimisha na kuzifahamu sheria za usalama barabarani pamoja na kuwa waangalifu wanapotumia barabara ili kujihakikishia usalama wao pamoja na watumiaji wengine kwa kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la ajali za barabarani.


No comments:

Post a Comment