Monday, April 30, 2018

Walimu 146 Wahitimu Mafunzo ya Awali ya Skauti Wilaya ya Hai


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Edward Ntakiliho akisisitiza jambo wakati akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya awali ya skauti kwa walimu wa shule za msingi na sekondari (hawapo pichani); hafla iliyfanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo tarehe 30/04/2018 (Picha zote na Adrian Lyapembile)


Na. Adrian Lyapembile
HAI

Wito umetolewa kwa walimu kuwa chachu ya tabia njema na mwenendo bora kwa kuishi maisha ya mfano kwa wanafunzi wao na jamii kwa ujumla katika kutekeleza majukumu ya kazi pamoja na kuwa wazalendo kwa kutanguliza mbele maslahi mapana ya taifa.


Akizungumza katika hafla ya kuwatunuku vyeti walimu wa shule mbalimbali za msingi na sekondari iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Edward Ntakiliho amesema halmashauri itaendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha kuwa shule zote za msingi na sekondari zinapeleka walimu kwenye mafunzo hayo na kupata wakufunzi wa skauti.


“Kuanzia sasa tunategemea walimu na wanafunzi wakiongozwa na mwalimu wa skauti watakuwa wazalendo kwa nchi, watakuwa watetezi wa mambo mema kwa jamii na kukemea vitendo viovu” ameongeza Ntakiliho.


Kwa upande wake Kamishna wa Skauti mkoa wa Kilimanjaro Bright Matola amesema kuwa lengo la mafunzo hayo kwa walimu ni kuwafanya wakawe mabalozi wazuri kwa wanafunzi wao katika vituo vyao vya kazi kwani kufanya hivo ni imani kuwa wanafunzi watakuwa wakakamavu kutokana na mafunzo watakayopata kutoka kwa walimu hao.


Aidha Matola amebainisha kuwa jumla ya walimu 146 wamehitimu mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti vyao hii leo ikiwa ni kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari za serikali pamoja na shule binafsi ambao wameitikia wito huo.


Akizungumzia ushiriki wa Wilaya ya Hai; kamishna wa skauti wilaya hiyo Upendo Fredrick amesema kuwa mafunzo hayo yatajenga walimu bora ndani ya wilaya huku akitoa wito kwa shule ambazo hazijapeleka walimu katika mafunzo hayo kufanya hivyo kwenye mafunzo yatakayoendelea kutolewa kwenye wilaya nyingine ikiwemo wilaya ya Siha itakayoanza mafunzo hayo mwishoni mwa wiki hii. 

Nao baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo wameeleza namna walivyofaidika kupata mafunzo lakini pia namna watakavyotumia ujuzi walioupata kusaidia jamii zao wanaporudi kwenye vituo vyao vya kazi.

Mwalimu Joel Mgelula wa shule ya Msingi Mbweera amesema kwenye mafunzo hayo wmejifunza ujasiri pamoja na jinsi ya kusaidia watu wanapopatwa na matatizo ikiwemo majanga ya moto na mengineyo huku mwalimu Mollel wa shule ya Msingi Kia ambaye anajivunia kujengewa uzalendo wa kuitetea nchi mahali popote na kwa wakati wowote atakapohitajika.

Mafunzo hayo yamefanyika kuitikia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alilolitoa kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya skauti nchini linalotaka kila shule iwe na kikundi cha skauti na kuwekewa msisitizo katika ngazi ya mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira.
Afisa Elimu Wilaya (Shule za Msingi) Deograsia Mapunda akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na wahitimu wa mafunzo hayo.

Baadhi ya Wahitimu wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi

Baadhi ya Wahitimu wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya awali ya skauti akipokea cheti chake kwa mgeni rasmi

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Kilimanjaro Bright Matola akiwa kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya awali ya skauti katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Kamishna wa Skauti Wilaya ya Hai Upendo Fredrick akiwa kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya awali ya skauti katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Kaimu Afisa Elimu Wilaya (Shule za Sekondari) Jafar Zaid akisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti walimu waliohitimu mafunzo ya awali ya skauti.



No comments:

Post a Comment