Monday, December 11, 2017

MAREKEBISHO YA SHERIA KUTOKOMEZA MIMBA ZA UTOTONI

Naibu Waziri George Kakunda akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Harambee alipofanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Hai.


Na. Adrian Lyapembile
HAI

Serikali imejipanga kufanya marekebisho ya sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 ili kukabiliana na ongezeko la matukio ya  mimba kwa watoto walio chini ya miaka 18 hasa wanafunzi.

Dhamira hiyo ya Serikali imebainishwa na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais TAMISEMI George Kakunda katika mkutano aliofanya na watumishi wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Amesema mabadiliko yatakayofanywa kwenye sheria hiyo ni pamoja na kuondoa dhamana kwa watuhumiwa wa matukio ya ubakaji na waliowapa mimba wanafunzi lakini pia washiriki katika kusababisha ndoa za utotoni ili kuepusha watuhumiwa kuharibu ushahidi wa makosa waliyotenda pale wanapokuwa uraiani.

Aidha ameitaka jamii kwa ujumla kushirikiana kupiga vita matukio ya mimba za utotoni  na kwa wanafunzi ambayo yameonekana kuongezeka kwenye mkoa wa Kilimanjaro na kubainisha kuwa wazazi wana mchango mkubwa katika kutokomeza matukio hayo kwani ni kesi chache zinazofikishwa mahakamani na nyingi hazitolewi hukumu kwa kukosekana ushahidi.

Amewataka walimu na watumishi wa umma kuwa mabalozi wa kuwaelimisha wazazi kuhusu malezi ya watoto na zaidi kujiepusha na namna yoyote ya ushiriki kwenye kuharibu ushahidi pale inapotokea mtoto amepewa mimba bali washiriki kuhakikisha haki inatendeka na wahalifu wanapata adhabu wanayostahili.


Wakati huohuo Naibu Waziri Kakunda amewataka watumishi wa umma kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kutunza rasilimali za nchi kwa kudhibiti matumizi ya fedha hasa kwenye ujenzi kwa kutumia wataalamu waliopo kwenye maeneo yao kwa mtindo wa ‘force account’ ambao umeonesha kuwa bora zaidi kwa miradi midogo ya ujenzi.

No comments:

Post a Comment