Na. Adrian Lyapembile
HAI
Watanzania wametakiwa kuiunga mkono serikali
katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo kwenye maeneo yao kwa kushiriki kulipa
kodi mbalimbali zilizowekwa kisheria huku wakitambua kuwa kodi ni msingi wa
maendeleo ya nchi hasa kwa wakati huu ambapo nchi inajizatiti kuelekea uchumi
wa wa kati kwa kuimarisha viwanda.
Wito huo umetolewa mapema leo Mei 23 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hasani Abass kwenye mahojiano na kituo cha Redio Boma Hai cha Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kuwatembelea maafisa Habari na Mawasiliano wa Sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Dkt. John Magufuli imejizatiti kuwahudumia na kuwatumikia wananchi
wake kwa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi katika maswala ya maji,
umeme pamoja na kufufua viwanda vidogo na vikubwa kwa lengo kuu la kuboresha
maisha ya Mtanzania mmojammoja nan chi nzima kwa ujumla.
“Niwaombe wananchi waendelee kuiunga mkono serikali
yao kuanzia viongozi waliopo kwenye ngazi ya wilaya yaani Mkuu wa Wilaya,
Wakurugenzi, Wabunge, Madiwani nikiamini kuwa viongozi wote hawa wana dhamira
ileile ya Mhe. Rais ya kuona mtanzania anaondokana na kero ambazo hazina msingi
wala hazina sababu ya kuwepo lakini pia viongozi waliopo niwaase waendelee
kutekeleza kazi zao kwa kasi kama ambavyo Mhe. Rais anataka ili wananchi waweze
kuona matokeo chanya”. Ameongeza Dkt. Abbas.
Aidha Dkt. Abbas amewataka wananchi kufuatilia kwa
karibu utendaji wa serikali ya awamu ya tano na kujionea hatua zinazopigwa
katika kuleta maendeleo ya nchi kwani kwenye kila sekta kuna kazi kubwa ya
kimageuzi inafanyika huku akitolea mfano sekta ya nishati inayoboreshwa kwa
utekelezaji wa miradi ya Kinyerezi I ambayo upanuzi wake ukikamilika utazalisha
megawati za umeme 185; mradi wa Kinyerezi II utakaozalisha megawati 240
umeshazinduliwa pamoja na mradi mkubwa wa Stigler’s Gorge ambao ni mradi wa
kihistoria utakaozalisha megawati 2100 za umeme ukiwa kwenye hatua ya uchambuzi
baada ya kutangaza zabuni.
Pamoja na miradi mingine, Dkt. Abbas amezungumzia utekelezaji
wa mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa itakayounganisha Tanzania na nchi jirani
ya Rwanda ambayo itaanzia Daresalam huku akibainisha kuwa treni hizo
zitaendeshwa kwa umeme huku serikali ikipiga hatua nyingine kubwa ya kutangaza
zabuni ya kuleta mabehewa na vichwa vya treni 1590 ambapo kati yake mabehewa
1560 yatakuwa ya kubeba mizigo ya aina mbalimbali na yaliyobaki yatakuwa ya
kubeba abiria.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano
Serikalini (TGCO) Paschal Shelutete amewakumbusha
maafisa habari wa Halmashauri jukumu lao kuu la kuwahabarisha
wananchi kuhusu maswala ya maendeleo na kuwataka wasiwe kikwazo cha utoaji
taarifa kwa wananchi bali wao wawe chachu
ya kufanikisha taarifa kuwafikia wananchi kuhusiana na utekelezaji wa kazi za
serikali katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wametekeleza vizuri
jukumu lao la kumsaidia Mhe. Rais katika juhudi za kuleta maendeleo nchini.
No comments:
Post a Comment